![]() |
photo by everystockphoto.com |
Nianze kuelezea tatizo
linalokwamisha watu wengi katika kufanya kazi na wazungu ukiachana na tatizo la
lugha. Ipo namna hii, kwa kawaida katika mahusiano yetu ya elimu, kazi na
biashara kibongo bongo ni kawaida sana kupeana ahadi zisizokamilika.
Ninapozungumzia ahadi naamanisha hata kule kukubaliana kukutana saa fulani
halafu mtu asitokee kwa muda mliokubaliana nako ni kuvunja ahadi. Ila kuna
kasumba nyingine mbaya sana ya kuahidi kufanya shughuli fulani au kumpatia mtu
kitu fulani siku fulani na wala usimpatie mtu husika au ukampatia ila kwa
kuchelewa tena baada ya kukumbushwa naye mara kwa mara. Hali hii wenyewe
tunaiita uswahili.
Uswahili huo upo katika
biashara, katika elimu , na hata makazini. Nimeishi na kufanya kazi kwa muda
mrefu na watu kutoka bara la Ulaya na Amerika ya Kaskazini hususani toka Marekani,
Uingereza na Ujerumani na kushuhudia jambo linalowapa shida sana katika
mahusiano yao na sisi waswahili ni huo uswahili kwakuwa pamoja na kuwa huko
kwao wapo wanaotokea kutotimiza ahadi nyakati fulani, ila kwa ujumla watu wengi
wakiwa katika mambo ya msingi katika elimu, biashara na kazi hutunza ahadi
wanazotoa.
Wazungu wanajifunza
toka wadogo kuwa ili ukubalike katika jamii inakupasa kumaanisha unachosema
utafanya, kwa maana ya kwamba kutokutimiza ahadi ya jambo ambalo ni wewe
mwenyewe ulisema ungefanya ni kujikanusha na kujionyesha mbabaishaji, usiyefaa
kuaminika, na hivyo watu watakugwaya kwenye mahusiano nawe kwa mambo ya msingi.
Pia wanajifunza
kutegemea wengine kutimiza wanayosema hivyo wao nao kupanga mambo yao kuendana
na ahadi na mipango wanayofanya na wengine. Wazungu wengi wana mazoea ya kuwa
na mipango ya muda mrefu, hata appointments (ahadi za kukutana na watu) huwa
wanaziandika katika diary au sehemu nyingine kama kwenye simu ili waweze
kukumbuka na pia kama itatokea kutaka kufanya appointment nyingine kwanza
hucheki orodha ya appointments ambazo tayari wamekwishaweka.
Kujifunza kwao kuheshimu
ahadi kunaendana sambamba na kuwahi au kufika kwa muda ule ule mliokubaliana
mkutane kwakuwa kutokufika kwa muda mliokubaliana ni kuvunja ahadi, na kuvunja
ahadi ni dalili ya kutokuthamini na kumheshimu mtu mwingine na muda wake.
Kinyume chao, sie bongo, wengi tumezoea kuwa ahadi ni maneno tuu na kuwa inawezekana tuu kutoa kisingizio cha kutotimiza ahadi husika bila tatizo. Ndio maana mtu hata kama anajua hatoweza kufanya jambo kwa muda fulani , yeye huamua kusema atafanya, ila itatokea kutokulifanya na huja na visingizio vya “maana” kujitetea kwa nini hakutimiza alilosema angefanya.
Sie kibongo bongo pia
wakati wa kukutana(appointment) tayari katika akili zetu tunakuwa
tumeshategemea kuwa mwingine atachelewa, na wala haitusumbui akilini kuwa
kutokufika kwa muda uliopangwa ni tatizo kwani daima mtu huja na sababu “nzito”.
Nimeshuhudia “waswahili”
kadhaa wakikosa fursa za kufanya mambo ya maana na wazungu kwakuwa wazungu husika
hawakuwa na muda wa kuvumilia kama wabongo tunavyovumilia huo uswahili. Wapo
wabongo ambao hutimiza makubaliano yao “kizungu” na hivyo wazungu wanaowapata
watu wa namna hii hudumu nao sana.
Hivyo kama unataka kazi
au mahusiano yenye tija na endelevu na wenzetu wengi wa nchi za magharibi,
jifunze kuwa mtu wa maneno yako. Usiahidi usichoweza kutimiza, hakikisha kabla
ya kukubali au kuahidi kufanya jambo fulani unachunguza mipango yako ya muda
mrefu, unachunguza changamoto zako na vikwazo ambavyo pengine vitakukwamisha
kutotimiza ahadi. Weka ahadi unazoweza kuzitimiza. Na kama inatokea jambo
ambalo hukulitambua mapema kama kikwazo mtaarifu mtu husika uliyemuahidi mapema
na sio kukaa kimya mpaka wakati wa ahadi au mpaka mhusika akuulize.
Hata wewe unaweza kuwa “mzungu”.
Hii inawezekana kwa kuanza kuamini kuwa unaweza kubadilika na kuwa hali ya “uswahili” si njia sahihi ya kuishi
kiungwana na si njia ya kuonyesha unawajali wengine. Thamini muda wa wengine,
thamini mipango ya wengine inayotegemea kutimiza ahadi zako, wapende na
kuwajali wengine , nawe upendo na kujali huko kutakurudia na utapata manufaa
kibao katika maisha yako.