Monday, May 11, 2015

JAMBO 1 LA MSINGI KAMA UNATAKA KUFANYA KAZI KWA MAFANIKIO NA MZUNGU

photo by everystockphoto.com
Nianze kuelezea tatizo linalokwamisha watu wengi katika kufanya kazi na wazungu ukiachana na tatizo la lugha. Ipo namna hii, kwa kawaida katika mahusiano yetu ya elimu, kazi na biashara kibongo bongo ni kawaida sana kupeana ahadi zisizokamilika. Ninapozungumzia ahadi naamanisha hata kule kukubaliana kukutana saa fulani halafu mtu asitokee kwa muda mliokubaliana nako ni kuvunja ahadi. Ila kuna kasumba nyingine mbaya sana ya kuahidi kufanya shughuli fulani au kumpatia mtu kitu fulani siku fulani na wala usimpatie mtu husika au ukampatia ila kwa kuchelewa tena baada ya kukumbushwa naye mara kwa mara. Hali hii wenyewe tunaiita uswahili.

Uswahili huo upo katika biashara, katika elimu , na hata makazini. Nimeishi na kufanya kazi kwa muda mrefu na watu kutoka bara la Ulaya na Amerika ya Kaskazini hususani toka Marekani, Uingereza na Ujerumani na kushuhudia jambo linalowapa shida sana katika mahusiano yao na sisi waswahili ni huo uswahili kwakuwa pamoja na kuwa huko kwao wapo wanaotokea kutotimiza ahadi nyakati fulani, ila kwa ujumla watu wengi wakiwa katika mambo ya msingi katika elimu, biashara na kazi hutunza ahadi wanazotoa.

Wazungu wanajifunza toka wadogo kuwa ili ukubalike katika jamii inakupasa kumaanisha unachosema utafanya, kwa maana ya kwamba kutokutimiza ahadi ya jambo ambalo ni wewe mwenyewe ulisema ungefanya ni kujikanusha na kujionyesha mbabaishaji, usiyefaa kuaminika, na hivyo watu watakugwaya kwenye mahusiano nawe kwa mambo ya msingi.

Pia wanajifunza kutegemea wengine kutimiza wanayosema hivyo wao nao kupanga mambo yao kuendana na ahadi na mipango wanayofanya na wengine. Wazungu wengi wana mazoea ya kuwa na mipango ya muda mrefu, hata appointments (ahadi za kukutana na watu) huwa wanaziandika katika diary au sehemu nyingine kama kwenye simu ili waweze kukumbuka na pia kama itatokea kutaka kufanya appointment nyingine kwanza hucheki orodha ya appointments ambazo tayari wamekwishaweka.

Kujifunza kwao kuheshimu ahadi kunaendana sambamba na kuwahi au kufika kwa muda ule ule mliokubaliana mkutane kwakuwa kutokufika kwa muda mliokubaliana ni kuvunja ahadi, na kuvunja ahadi ni dalili ya kutokuthamini na kumheshimu mtu mwingine na muda wake.

Kinyume chao, sie bongo, wengi tumezoea kuwa ahadi ni maneno tuu na kuwa inawezekana tuu kutoa kisingizio cha kutotimiza ahadi husika bila tatizo. Ndio maana mtu hata kama anajua hatoweza kufanya jambo kwa muda fulani , yeye huamua kusema atafanya, ila itatokea kutokulifanya na huja na visingizio vya “maana” kujitetea kwa nini hakutimiza alilosema angefanya.

Sie kibongo bongo pia wakati wa kukutana(appointment) tayari katika akili zetu tunakuwa tumeshategemea kuwa mwingine atachelewa, na wala haitusumbui akilini kuwa kutokufika kwa muda uliopangwa ni tatizo kwani daima mtu huja na sababu “nzito”.

Nimeshuhudia “waswahili” kadhaa wakikosa fursa za kufanya mambo ya maana na wazungu kwakuwa wazungu husika hawakuwa na muda wa kuvumilia kama wabongo tunavyovumilia huo uswahili. Wapo wabongo ambao hutimiza makubaliano yao “kizungu” na hivyo wazungu wanaowapata watu wa namna hii hudumu nao sana.

Hivyo kama unataka kazi au mahusiano yenye tija na endelevu na wenzetu wengi wa nchi za magharibi, jifunze kuwa mtu wa maneno yako. Usiahidi usichoweza kutimiza, hakikisha kabla ya kukubali au kuahidi kufanya jambo fulani unachunguza mipango yako ya muda mrefu, unachunguza changamoto zako na vikwazo ambavyo pengine vitakukwamisha kutotimiza ahadi. Weka ahadi unazoweza kuzitimiza. Na kama inatokea jambo ambalo hukulitambua mapema kama kikwazo mtaarifu mtu husika uliyemuahidi mapema na sio kukaa kimya mpaka wakati wa ahadi au mpaka mhusika akuulize.


Hata wewe unaweza kuwa “mzungu”. Hii inawezekana kwa kuanza kuamini kuwa unaweza kubadilika na kuwa hali  ya “uswahili” si njia sahihi ya kuishi kiungwana na si njia ya kuonyesha unawajali wengine. Thamini muda wa wengine, thamini mipango ya wengine inayotegemea kutimiza ahadi zako, wapende na kuwajali wengine , nawe upendo na kujali huko kutakurudia na utapata manufaa kibao katika maisha yako.

0 comments:

Post a Comment