Monday, March 30, 2015

KINACHOWAKWAMISHA WENGI KATIKA KUTAFUTA MSAADA

Iwe unatafuta msaada wa kifedha, ushauri au ushirikiano katika lile unalolifanya ni vema ukatambua namna bora ya kuelezea unalolihitaji kwa mtu au taasisi husika. Pia haitoshi kujieleza unahitaji nini, inakupasa uwe mtu ambaye kweli unastahili kusaidiwa.  Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayokwamisha wengi katika kuomba msaada:
Kushindwa kujieleza kwa ufasaha
Wewe ndie unayejua haswa unachohitaji, hivyo inakupasa kufafanua kile unachokifanya, wapi umekwama, na nini unahitaji huyo mtu mwingine afanye, na afanye kwa kiwango gani, na kwanini akusaidie wewe. Mfano mara nyingi nimepokea meseji mtu ananiambia “Bro naomba nitafutie schorlaship”.  Hili si ombi lililojitosheleza kwani , schorlaship ni swala pana, ni schorlaship ya nini, wapi, kwanini unastahili kupata schorlaship n.k. Kama wewe unayeomba unashindwa kutumia muda wa kutosha kufafanua unalohitaji, kwanini mtu mwingine atumie muda wake kujadiliana nawe ili ajue haswa unachohitaji. Ni muhimu kuonyesha kweli una juhudi katika hicho unachokitafuta.

Kutokuwa na mahusiano mazuri 
Mara nyingi mtu anayeweza kukusaidia ni yule anayekuthamini na kukufahamu. Mtu hawezi kukusaidia kama taswira yako kwake ni mtu usiyeaminika, usiyejitambua na usiyemheshimu na kumjali au kujali wengine. Ni vizuri basi kuwa na mahusiano mazuri na huyo unayetarajia kuomba msaada kwake, na pia ujenge taswira nzuri kwa jamii kwa kufanya mambo ya msingi.

Kutokutoa mrejesho 
Unapopata msaada kumbuka kwanini mtu huyo alikusaidia kwa mara ya kwanza. Sio tuu kwakuwa uliomba, ila amini mtu huyo anahitaji kujua tokeo la msaada wake. Wengi wanaposaidiwa huacha kueleza matokeo ya msaada waliopewa. 

Kutotumia vizuri msaada  
Ulimuanisha mtu aliyekupa msaada ulikuwa kweli mwenye kuhitaji huo msaada ndio maana ukapewa, hata hivyo kidogo ulichosaidiwa umeenda kitumia tofauti. Kwanini huyo mtu awe na imani akikusaidia tena, msaada wake utaenda kutumika ipasavyo.

Kutokuonyesha wanastahili kusaidiwa 
Kwa mtu anayeweza kukusaidia kwake ni muhimu kujua kama kweli unastahili kupokea huo msaada wake kwani si unajua hiyo ni mali iwe ni muda wa kukushauri au ni pesa za kufanyia biashara au shule. Sidhani kama mtu unayemuomba msaada anawaza kupoteza tuu msaada wake. Na njia ya yeyé kujua kama hatopoteza msaada wake ni kujua kuwa wewe unastahili kusaidiwa. Vitu anavyoweza kuangalia ili kujua kama unastahili kusaidiwa ni pamoja na uaminifu , ujuzi, uzoefu wako,  taswira yako , mahusiano yake na yeye, n.k

Kuogopa kuomba msaada
Kuna baadhi ya watu huogopa kujitokeza kuomba msaada, kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutojiamini, kuogopa au kushindwa kujieleza, na wakati mwingine hata kutokuamini kama wanaweza kusaidiwa.


HITIMISHO: Je, wewe ni miongoni mwa wenye matatizo yaliyotajwa hapo juu ? Tuzungumze tuone tunalitatuaje tatizo hilo. Like ukurasa wetu wa Facebook, na unitumie meseji.

0 comments:

Post a Comment